Ifuatayo ni hotuba ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli, mgombea wa CCM kwa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akitambulishwa rasmi mjini Dodoma, tarehe 12 Julai 2015. Awali ya yote, napenda nichukue fursa hii adhimu sana, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote yaliyofanyika hata kuniwezesha leo hii kuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi. Namshukuru kwanza, kwa kutufikisha wote hapa tukiwa buheri wa afya. Namshukuru pia, kwa kutusimamia vizuri, kwa Usalama na Amani toka kuanza kwa mchakato huu hadi hapa tulipofikia. Tunazidi kumuomba aendelee kutusimamia mpaka ushindi utakapopatikana.
Naomba nirudie tena kuwashukuru kwa moyo wa dhati Kamati Kuu, Wajumbe wa Halmashauri Kuu na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa heshima kubwa mliyonipa kuipeperusha bendera ya CCM katika kinyang’aniro cha Urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Nakosa maneno sahihi na muafaka ya kuwashukuru. Ahadi yangu kwenu ni kwamba sitowaangusha kamwe. Nitalipa fadhila hii, kwa kuinadi na kuisimamia vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2015 na kuitekeleza kwa makini kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania ili tuendelee kukiweka Chama chetu kwenye nafasi ya ushindi daima. Asanteni sana.
John Pombe Magufuli na Jakaya M. Kikwete |
Naomba nirudie tena kuwashukuru kwa moyo wa dhati Kamati Kuu, Wajumbe wa Halmashauri Kuu na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa heshima kubwa mliyonipa kuipeperusha bendera ya CCM katika kinyang’aniro cha Urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Nakosa maneno sahihi na muafaka ya kuwashukuru. Ahadi yangu kwenu ni kwamba sitowaangusha kamwe. Nitalipa fadhila hii, kwa kuinadi na kuisimamia vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2015 na kuitekeleza kwa makini kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania ili tuendelee kukiweka Chama chetu kwenye nafasi ya ushindi daima. Asanteni sana.
Niwashukuru sana viongozi wa wana CCM wa Dodoma kwa kuandaa hafla hii ya kuzungumza nanyi na kupitia kwenu kwa wananchi wote wa Tanzania kwa mara ya kwanza tangu nilipoteuliwa na Chama leo asubuhi.
Najua matarajio ni makubwa sana. Natambua, Watanzania wote, wanataka misingi ya amani na umoja wetu iliyojengwa na waasisi wa nchi yetu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume na kuimarishwa na kuendelezwa na viongozi waliofuatia wa Jamhuri ya Muungano na Marais wa Zanzibar inaendelea kudumishwa. Wanataka kuona Muungano wetu na umoja baina ya watanzania unaendelea kudumishwa bila kujali dini zao, rangi zao, makabila yao, wala mahali watokako.
Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kwamba mkikichagua Chama cha Mapinduzi nitasimamia na kupigania misingi hii kwa nguvu zote, kwa moyo wote na kwa kutumia vipaji vyote nilivyojaliwa na Mwenyezi Mungu ili nchi yetu iendelee kuwa moja, Muungano wetu uzidi kustawi na kuhakikisha wanatanzania wote wanaendelea kuishi kwa umoja na mshikamano.
Pili, Watanzania wanataka maendeleo ya haraka. Katika hili natambua kwamba kila Mtanzania anao uwezo wa kujiletea maendeleo. Bahati nzuri tayari misingi ipo. Nitafanya jitihada ya kukidhi kiu yao hii kwa kuendeleza misingi sahihi iliyojengwa katika awamu zote nne zilizonitangulia. Nyote ni mashuhuda wa kazi nzuri iliyofanywa na mafanikio makubwa yaliyopatikana kama yalivyoelezwa bayana na Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 09 Julai, 2015.
John Pombe Magufuli |
Nitayaendeleza kwa umakini, uhodari, juhudi na maarifa ya hali ya juu, ili sasa nchi yetu ipae kuelekea kwenye maendeleo ya juu kwa pato la nchi na pato la kila mmoja wetu. Tupunguze umaskini kwa kasi kubwa zaidi. Nafarijika kwamba Ilani ya Chama chetu inanituma hivyo, nitaitekeleza kwa umakini wa hali ya juu kabisa kwa manufaa ya nchi yangu na ya kila Mtanzania.
John Pombe Magufuli |
Tatu, natambua kwamba usalama wa raia na mali zao, na ulinzi wa uhuru na mipaka ya nchi yetu ndiyo uhai wa taifa letu. Hatutakuwa na mchezo na mtu yoyote atakayejaribu kuhatarisha uhuru na mipaka yetu. Tutaendelea kutekeleza Sera za CCM za kuboresha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili viweze kutekeleza wajibu wao huo kwa ufanisi mkubwa zaidi na viendelee kuheshimika ndani na nje ya nchi, viendelee kudumisha usalama wa wananchi wa Tanzania pamoja na mali zao.
Nne, natambua kuwa Watanzania wote; vijana, wanawake, wazee, wanaCCM na wasio wana CCM, wote wana matumaini makubwa na Chama cha Mapinduzi. Kwa watoto, tunajua wanataka kupata huduma bora hususan za elimu na afya. Kwa vijana, matumaini yao ni kuona juhudi za utatuzi wa changamoto zinazowakabili zikiwamo ukosefu wa ajira zinafanyika kwa kasi kubwa zaidi. Kwa akina mama, vijana na wazee matarajio yao ni kupata huduma zilizoimarika kama vile afya, upatikanaji wa maji, umeme hasa vijijini, kilimo bora na chenye tija, masoko kwa ajili mazao ya kilimo na mazao mengine yatokanayo na sekta mbalimbali, usafiri wa uhakika wa barabara, reli, anga na majini.
John Pombe Magufuli - Kushoto Ili haya yote yaendelee kutekelezwa vizuri na kwa ufanisi mkubwa Watanzania wanayo Imani kubwa na matumaini kwa Chama Cha Mapinduzi. Chama chenye uwezo wa kuyaendeleza haya. Ni katika Imani hii basi, naamini kuwa mwezi Oktoba, CCM itashinda kwa kishindo na kuendeleza hatamu ya uongozi wa nchi yetu kwa Awamu ya Tano. Napenda niwahakikishie kuwa, nikichaguliwa kuwa Rais wa nchi yetu, kazi yangu kubwa ni kuhakikisha Ilani inatekelezwa kikamilifu na kuongeza kasi ya maendeleo kwa Watanzania wote, vijana kwa wazee, wanawake, watoto wetu na nchi kwa ujumla. Tunachohitaji ni umoja miongoni mwetu wana CCM kama kauli mbiu yetu inavyosema Umoja ni Ushindi. Naomba viongozi na wanachama wa CCM tuiishi kauli hii kwa matendo.
CCM iko tayari kwa mageuzi ya uhakika na ya haraka kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Nitawauliza? Kwa mageuzi ya uhakika na maendeleo ya haraka kwa wote tuchague chama gani? CCM, kumbe mnajua.
Leo ni siku muhimu katika historia ya chama chetu, na mimi mwenyewe binafsi. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele yenu nikiwa salama na afya njema kutoa shukrani zangu za dhati kutoka chini ya sakafu ya moyo wangu, kwenu wajumbe wa Mkutano Mkuu, Wajumbe wa NEC, CC na Baraza la Wazee la ushauri, kwa kuniamini na kunikabidhi bendera ya chama chetu niipeperushe kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
John Pombe Magufuli |
Nakumbuka Mzee wangu Ali Hassan Mwinyi akiwa katika nafasi kama yangu mwaka 1985, alisema “nimehemewa” sasa natambua kwa nini alisema vile. Miye nasema nimehemewa sana. Hii ni kwa sababu imani mliyonipa ni kubwa, dhahiri na thabiti.
Jana, (Jumamosi) wakati naomba kura zenu nilisema “nitumeni nami nitawatumikia”. Nawashukuru sana kwamba mmekubali kunituma, tena kwa kura za kishindo sina cha kuwalipa isipokuwa kusema asanteni sana tena sana tena sana na kuwaahidi kwamba nitawatumikia kwa nguvu zangu zote, kwa moyo wangu wote na kwa kutumia vipaji vyote nilivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Mmenipa heshima kubwa. Naahidi kuilipa heshima hiyo kwa kuinadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kufafanua Sera za CCM mpaka zieleweke na kukubalika na kila mmoja. Kazi hiyo nitaifanya pamoja nanyi nyote mpaka tupate ushindi wa kishindo, tena ushindi wa mafuriko.
John Pombe Magufuli - Juu ya gari |
Kinachotakiwa ni umoja na mshikamano wetu ninawaomba wenzangu wote 38, viongozi wa CCM ngazi zote na wanachama, mashabiki na wapenzi wa CCM tuungane pamoja kuhakikisha kwamba chama chetu kinapata ushindi. Tudhihirishe kauli mbiu yetu ya umoja ni ushindi kwa vitendo. Nafurahi sana na kujivuna kwamba napokea kuipeperusha bendera ya Chama cha Mapunduzi ambacho ni imara chenye wanachama wengi na viongozi imara na mahiri na madhubuti, wenye msimamo, mshikamano na wenye ari na hamasa ya hali ya juu. Chama ambacho ni imara kwa muundo wake na bora kwa sera zake.
Chama ambacho kimeliletea Taifa letu heshima kubwa ndani na nje ya nchi. Chama ambacho kina misingi imara ya kupata viongozi na kubadilishana uongozi kwa kufuata Katiba na taratibu za demokrasia ndani ya chama. Chama kilichokomaa. Chama kilicholelewa na kujengwa na miamba ya uongozi wa nchi yetu. Kuanzia na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi, Mzee wetu William Benjamin Mkapa na Mzee wetu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (Ingawa unaonekana bado kijana ukishastaafu Urais we ni mzee wetu tu).
John Pombe Magufuli - Kushoto |
Sote tunaona mchakato huu ulivyofanyika kwa busara kubwa. Tumeona pia mchakato wenye ushindani mkubwa kama huu ulivyoendeshwa na kumalizika salama salimin kwa utulivu na upendo, tunatoka hapa tukiwa wamoja, chama kimoja na mtandao wetu wa ushindi ni mmoja, yaani CCM. Waliotegemea kwamba chama chetu kingetoka hapa kimefarakana au kimemeguka sasa wanahaha. Kura mlizonipigia zinathibitisha ukweli huu. Kweli CCM ni chama imara ni viongozi wake mahiri, thabiti.
Napenda kuwahakikisia nitazienzi tunu hizi adimu na adhimu za Chama chetu, nitafanya kila jitihada kuzitetea, kuzifafanua na kuzilinda katika chaguzi ili nami pamoja nawe tuwe sehemu ya historia nzuri ya Chama chetu ya kuendelea kushika uongozi wa nchi yetu. Naomba nimalize kwa kuwashukuru tena wote mliosaidia kufanikisha mchakato huu ulioniwezesha mimi kuteuliwa kupeperusha bendera ya Chama chetu katika Uchaguzi Mkuu ujao. Nasema asanteni sana sana.
Mungu kibariki Chama chetu, Mungu Ibariki CCM. ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
BREAKING NEWS! "Don’t Wear Underwear to Church!" Pastor says!
Comments
Post a Comment